Wednesday, January 11, 2012

NDOA NA WANAWAKE


Wapendwa wangu leo nataka tuongee kidogo, nimeona ni vizuri kama tutashauriana pia ili tuone kama inawezekana kufanya hivyo mikasa kwenye ndoa zetu isitokee.
Katika mikasa mingi sana inawahusisha wanandoa, hasa wanawake,  mara mume wangu nimemfumania, mara mume wangu kiburi, mara mume wangu mchafu na mengine mengi, lakini je hamuwezi ninyi kama kina mama kuangalia ni jinsi gani mnaweza kufanya ili kuzuia? na pale yanapotokea basi iwe imebidi yatokee?ila ninyi msiwe chanzo.
Mshauriane kwa pamoja, mfanye nini ili mpunguze hii kasi ya machafuko kwa wanandoa, nina amini kabisa kama kila mtu ataplay part yake kama mama mwenye hekima basi 80% ya ndoa zetu  zitakuwa zimepona.

(i) KUNUNA KUSIPITILEZE.

Kununa imo, lakini sio nongwa jamani, mtu ukinuna basi ndio lo!! Mwezi mzima, sasa tujiulize mnaponunia waume zenu mwezi mzima mnategemea nini???
Kama anakuhitaji kifamilia zaidi wewe si atapata nafasi ya kutoka nje? Maana akirudi home anaona kero, mama kanuna, tena wengine bila hata haya wanawambia watoto baba akija msimuamkie mkalale, kha! Baba lazima ajiulize hivi kuna haja gani ya kuwahi nyumbani, bora nikae bar nileweeeeeee, matokeo yake anaanza kurudi usiku amechoka baba wa watu,  na anarudi tu! kutimiza wajibu.

Pale inapobidi kukasirika,  yes! Show him kwamba hapa umekosea, ili nae ajuwe asikupande kichwani,  na kama umeamua  kumtingisha kwa kununa basi huo mnuno wako uwe na kiasi, sio ndio kila akikusemesha umevuta mdomo, jamani msipoangalia  mtazipoteza ndoa zenu wakati bado mnazitaka.

Mbali na hilo tukumbuke katika yale mambo serios lazima tuwe serios kweli, mfano kuna mmoja alisema ameambiwa aache kazi,  dada huyu anaweza kukaa namumewe kwa upole na upendo akamwambia tu! kwanini niache kazi? asikilize hizo sababu, ili nae apate muda wa kujitetea, pengine kazi inamtia kiburi anasahau majukumu yake kama mama ?
Pengine baba hapati huduma inavyostahili ? pengine housegirl ndio kila kitu ? hadi kusema hivyo lazima kuna reason, tusikimbilie kusema ondoka, au achana nae,  we! usipime, mume mtamu jamani, mume anauma asikwambie mtu, ifike kipindi mjichunguze je mna mapungufu gani ninyi kina mama kwa upande wenu, kabla hamjaanza kulaumu waume zenu.

Kinamama mnapoishi na waume zenu kwenye ndoa, baada ya muda huwa  mnajenga mazowea, ambayo sometimes yanakuwa hayajengi bali yanabomoa, mazowea ya aina hii huleta kiburi ambacho kwa namna moja ama nyingine kina madhara makubwa sana, unakuta mwanamke anamdomo mchafu afadhali ya choo, anamjibu mumewe majibu machafu hata mbele za watu /watoto wao.

Kitu ambacho ni kibaya sana, sababu wale watu wanaowazunguka ninyi wawili watajua tofauti zenu, na mtatiana aibu sana maisha yenu yatakuwa nje, kila mtu atawaona vihoja kuanzia watoto hadi majirani, lo! mbadilike jamani.

Mume anataka kuheshimiwa, ili na watoto wajifunze heshima kupitia kwa mama yao, lakini utakuta mtu akiudhiwa anaropoka hovyo maneno makali ambayo baada ya ugomvi wao kuisha inageuka kuwa aibu kwake.

ii) (MALIZENI TOFAUTI ZENU CHUMBANI KWENU )

Turejee mafundisho ambayo wengi wenu huwa mnapewa kwenye Kitchen Party zenu, malizeni chumbani migogoro yenu, au hata ukimnunia  basi watoto wasijue, au majirani, mwingine akinuna basi hata kama ni maji ya kuoga haweki, kama ni nguo ya ndani ndio hatafua tena, kama ni chakula ndio hatamuandalia tena, jamani jamani, mjitahidi jamani ndoa ni ghali.

Wanaume ni kama watoto wadogo, utakavyompenda mwanao na kumuweka karibu na wewe ndio atakupenda sana, lakini mtoto ukimfokea fokea tu atakuogopa na kukuchukia, ndio kama waume zenu, mkiwaweka karibu watakuwa marafiki kabisa.

NDOA TAMU jamani asikwambie mtu, tusifikiri ndoa inaweza kuvunjika kwa urahisi. Sometimes mkikosana, jaribu kukumbuka mmetokea wapi?? Kumbuka siku yako ya harusi, kumbuka mapenzi mliyo kuwanayo kipindi kileeee, halafu uya apply kwenye ndoa yako sasa.

Ndoa ina heshima yake kama mtaheshimiana, na hata kama mtapishana basi mmoja lazima akubali kushuka, ukijishusha mwanamke hutoonekana mjinga kama wengi mnavyofikiria, bali utaonekana mke mwenye busara asiyetaka kuibomoa nyumba yake kwa mikono yake, KUJISHUSHA ni dawa moja nzuri sana,  hata kama hujakosea, kwani ukikaa kimya au kama unamueleza ukweli yeye haelewi, no need kupigizana kelele weeeee, NI KUJISHUSHA TU ndio dawa pekeee.


MWISHO

Monday, January 9, 2012

UJASILIAMALI

Biashara ya kuku wa kienyeji inavyoweza kukuondolea umasikini.

Na McDONALD MASSE

Watu wengi wamekuwa wakifikiria kuhusu namna ya kujikwamua kutoka kwenye umasikini.Leo hii nitawaelezea kuhusu biashara ya kufuga kuku wa kienyeji ambavyo inaweza kukukwamua kutoka kwenye umasikini. Lengo kuu ni kuwawezesha watu kutengeneza ajira kwao binafsi na watu wengine.
Takwimu za uzalishaji (kutaga, kuangua na kukuza kuku)
Utafiti uliofanywa na Dr. John Bishop kwa msaada wa shirika la kitaifa la utafiti wa kilimo nchini Equador na Chuo kikuu cha Florida nchini Marekani, umeonyesha kuwa ; Kama kuku akitunzwa vizuri kutokana na mbinu bora za ufugaji, anaweza Kuongeza uwezo wa kutaga mayai kutoka mayai 10 hadi mayai 12 kwa mwezi. Kwa mfano ukiwa na kuku 12 na jogoo 1 waliolishwa kilo 1 ya nafaka kila siku unaweza kuuza dazani 10 za mayai kila mwezi ambayo ni sawa na mayai 4 kila siku.
Jee unapenda kutajirika kwa kufuga na kuuza kuku?
Angalia mchanganuo wa mahesabu mapato yako yatakuwa kama ifuatavyo, Kwa kipindi cha miaka 2. K wa mtaji wa Sh. 500,000/= kama una eneo la eka 1 na mabanda ya kutosha kiasi cha kuku 10,000. Ukianza kwa kufuga kuku 25 ( kuku 20 na jogoo 5) ambao utawanunua kwa Sh. 250,000.00. Hao kuku 20 wakianza kutaga vifaranga 10 kila mmoja wataangua vifaranga 200 watunze vizuri katika vifaranga hao tuchukulie majike yanaweza kuwa 150 ambao ndani ya miezi 6 au zaidi nao wataanza kutaga. Kipindi hicho utakuwa na kuku (200+ 25 =225.) Baada ya hiyo miezi 6 kuku watakaotaga ni 170 kila mmoja akipata vifaranga 10 mpaka mwisho wa mwaka utakuwa na kuku (1700+20+55=1775) ukiuza kuku 1,000 kwa bei ya Tshs. 10,000 utapata Tshs. 10,000,000/=. Mwaka wa 2 majike 775 yakiangua vifaranga 10 kila mmoja utakuwa na kuku 7,550 mwisho wa mwaka ukiuza kuku 3,000 kwa bei ya Tshs. 10,000 utapata Tshs. 30,000,000/= Hesabu hizi ni kwa makadirio ya chini sana kwani kama nilivyoelezea hapo juu kuku mmoja kama atatunzwa vizuri anaweza kuataga mayai kati ya 10 hadi 12 kwa mwezi.
.Kuku wa kienyeji wamekuwa wakifugwa kwa wingi vijijini kwa malengo ya kupata nyama na mayai kwa ajili ya familia husika na kwa ajili ya kupata pesa za kujikimu. Kuku na mayai ya kienyeji yana faida kubwa kiafya kutofautisha na kuku wakisasa ambao hukuzwa kwa kemikali. Idadiya kuku Tanzania inakadiriwa kuwa na jumla ya kuku Milioni 34 wanaofugwa na takribani 60.5% ya kaya zinazojishughulisha na kilimo. Hata hivyo uzalishaji wake umebaki kuwa duni kutokana na changamoto za wafugaji zifuatazo; Utunzaji duni , Udhibiti mdogo wa magonjwa, lishe duni, makazi duni, Uzaliano wa karibu, Teknolojia duni, Kukosekana kwa mtazamo/mwamko wa kibiashara.
Faida ya kufuga kuku wa kienyeji.
Ufugaji wa kuku wa kienyeji una manufaa mengi kwa mfano; Kuku hutumia eneo dogo kuliko wanyama wengine wa kufugwa, pia hutumia chakula kidogo hivyo ufugaji unaweza kuendeshwa bila kutumia mtaji mkubwa. Kuku wanaweza kupewa mabaki ya chakula pamoja na vyakula vya kujitafutia kama vile wadudu,mbegu na majani. Kazi za usimamizi wa kuku zinaweza kufanywa na mama na watoto. Kuku na mayai humpatia mfugaji chakula bora na kumuongezea mapato. Pia mfugaji ni kama mtu aliyewekeza fedha zake benki au kwenye kitegauchumi kingine ambapo kuku huweza kuongezeka kutokana na kuku kutaga na kuangua vifaranga kama faida inavoongezeka benki na kwenye vitegauchumi vingine. Mfugaji ni sawa na mtu aliyeweka akiba benki kwani akipata shida anaweza kuuza kuku na kulipa ada, mahari matibabu ya hospitali pamoja na shida zingine. Kuku wa kienyeji anasaidia kusafisha mazingira kwa kula wadudu na kuongeza rutuba kwa mbolea inayotokana na kinyesi cha kuku ambacho hakina kemikali. Mbolea hii ni nzuri sana na kama inazalishwa kwa wingi inaweza kuwa chanzo kingine cha mapato kwa mfugaji wa kuku. Kuna mjasiriamali ninayemjua anafuga kuku wengi anazo tani nyingi za mbolea hii na anauza mbolea ya mavi ya kuku kwa Sh. 600 kwa kiloba cha kilo 50. Kuku wa kienyeji ana uwezo mkubwa wa kuhimili magonjwa, hutaga mayai na kutunza vifaranga badala ya kutumia mashine. Kuku wa kienyeji anaweza kuishi nchi yoyote duniani bila kuathiriwa na hali ya hewa.
Aina za magonjwa ya kuku na jinsi ya kukinga magonjwa.
Wapatie chanjo kuku wako kwa afya bora. Wapatie kinga mara kwamara kila baada ya miezi 3. Magonjwa yafuatayo ndiyo huwa yanawashambulia kuku.
New castle
Dalili za ugonjwa huu ni kuku kushindwa kupumua, kukohoa na kutokwa na mate,kuwa na kinyesi cha rangi ya kijani, ugonjwa huu hauna dawa. Chanjo hutolewa machoni kwa njia ya matone.
Minyoo.
Dalili za mionyoo ni kuku kukosa hamu ya kula uzalishaji wa mayai kupungua. Ukiona dalili hizo waone wataalamu wa mifugo upate dawa.
Wadudu.
Utitiri husumbua kuku, kwa kuwasababisha kukosa usingizi,ngozi kuharibika,huathiri uzalishaji wa mayai. Ukiona dalili hizi wasiliana na wataalamu wa mifugo upate dawa.
Magonjwa ya mapafu.
Huathiri sehemu za kupitishia hewa na kuwa na sauti ya kukoroma. Hali hii hupunguza uzalishaji wa mayai na uzito wa kuku kupungua. Ukiona dalili hizi wasiliana na wataalamu wa mifugo upate dawa.
Mambo mengine unayopaswa kuyajua kama mfugaji wa kuku
Inapokuja katika ufugaji wa kuku wa kienyeji ,mbinu inayotumiwa kijijini ile kuku huachwa azurure katika boma bila uchungaji ama na uchungaji mdogo.Kuna matatizo mengi ambayo kuku hukutana nayo. Kuku halishwi vyema kwani hula masalio ya.chakula na mabaki mengine wanayoyapata. Vifaranga wadogo huachwa washindanie chakula na kuku wakubwa na huwa nyama rahisi kwa wanyama wanaowinda na kula nyama na husambaza magonjwa. Kuku hawapati maji ya kutosha na hawana mahali pa kujisetiri dhidi ya upepo na mvua ama kuwaweka salama dhidi ya wanyama wanaowinda na kula nyama bila kusahau wezi. kuku hutaga mayai ardhini na yanaweza kuharibiwa kwa urahisi na kuliwa na wanyama wengine. Sio kawaida kuku kupewa chanjo na matibabu dhidi ya magonjwa na vimelea. Matokeo ni kuku wengi huwa wagonjwa na hukua pole pole,hutaga mayai machache na nyama kidogo.
Ili kuhakikisha mapato mazuri kutoka kwa kuku wako,fanya yafuatayo:
Kuwapatia kuku mgao mzuri wa vyakula tofauti na maji safi.Kutemeana na kipindi cha mwaka,wataweza kujitafutia chakula kwa kukwaruza ardhi katika boma. Wapatie chakula cha ziada ili kuku waongeze uzani na kuku watage mayai mengi zaidi. Walishe vifaranga na chakula kilicho na protini kama mchwa ili wakue kwa haraka na wawe na afya. Wajengee kuku mahali penye giza na patulivu ambapo wanaweza kutaga mayai yao.Kuku huhitaji kujisikia wakiwa salama kutoka kwa wanyama wanaowinda na kula nyama na wapita njia. Kama kuku watasumbuliwa mara kwa mara watakuwa wakiviacha viota vyao na hii huathiri uanguaji wa mayai. Ikiwa nia yako ni utoaji wa mayai,ni vizuri kufuga kuku wa kike pekee.Jogoo mmoja anaweza kufugwa aangalie wanyama wanaowinda na kula nyama na kuwahudumia kuku.Wakati jogoo wa ziada wanapofikia umri wa kuuzwa,wanafaa kuuzwa,kuchinjwa ama kutolewa kama zawadi kuzuia jogoo kula chakula ambacho ni adimu na kupigana na kuwataabisha kuku. Ukubwa wa kundi unafaa kuafikiana na ukubwa wa nyumba au banda ,kiasi cha chakula unachoweza kununua na raslimali za chakula katika maeneo yanayokuzunguka. Usinunue kuku kutoka katika vyanzo ambavyo havijathibitiwa haswa vipindi milipuko ya magonjwa ni kawaida kwa sababu wanaweza kusambaza magonjwa kwa wengine. Toa chanjo mara kwa mara kulingana na ushauri wa watoaji chanjo na madaktari wa wanyama wa nyumbani. Vifaranga wachanga wanapaswa kuchanjwa dhidi ya magonjwa ya kawaida ya kuambukizana wakifika umri wa wiki 2-3.
Ikiwa kuku watataabika kutoka kwa ugonjwa sugu unapaswa:
1. Kuita daktari wa wanyama
2. Kumtenga kutoka kwa wengine
3.Kuku anafaa kuuliwa mara moja kwa kutegemea jinsi ugonjwa ulivyo mzito na
anafaa kuchomwa ama kuzikwa katika kina kirefu ili kuzuia mbwa na wanyama wengine kuwachimba na kusambaza ugonjwa.
Angalia ni kuku wangapi wana dalili za kutaka kuangua mara moja kwa mwezi na uwapatie matunzo ya ziada.
MWISHO

Sunday, January 8, 2012

SOMA HIZIIIIIIIIIIIIIIIII






HABARI KWA UFUPI KUTOKA MATAIFA MBALIMBALI.

Jumuia ya nchi za Kiarabu imetoa wito kwa serikali ya Syria na makundi yenye silaha yaache haraka kutumia nguvu dhidi ya raia.

Mawaziri wa mashauri ya nchi za nje wakikutana mjini Cairo, wameamua kuwa ujumbe walioutuma Syria kuchunguza hali, uendelee na kazi yake, ingawa wapinzani wamelalamika kuwa hausaidii kumaliza fujo.
=================
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amehutubia maelfu ya wafuasi wa chama cha  ANC, katika sherehe zilizomalizika jana za kuadhimisha miaka 100 tangu chama hicho kuundwa - chama kikongwe kabisa cha ukombozi barani Afrika.

Bwana Zuma amesema  siku hiyo ni siku ya furaha kwa watu wa Afrika Kusini, ambao waliangamiza ukoloni na ubaguzi wa rangi, kwa kusaidiwa na Afrika na ulimwengu.

Nelson Mandela hakuweza kuhudhuria kwa sababu ni dhaifu.

=========================
Rais Omar al-Bashir, ambaye anazuru Libya, amesema anaweza kuisaidia Libya kuwafanya wapiganaji wa zamani kusalimisha silaha na kuwajumuisha kwenye jeshi na polisi.

Wapiganaji wanaopingana nchini Libya wanashindana kuhodhi madaraka baada ya kuondoshwa kwa Kanali Gaddafi.

Rais al-Bashir amewaambia wenyeji wake kwamba ana uzoefu wa kuwaleta pamoja wapiganaji.

NA HUO NDIO MWISHO WA HABARI KWA UFUPI KUTOKA MATAIFA MBALIMBALI NA KWA HABARI KWA UFUPI USIKOSE KUJIUNGA NASI TENA ITAKAPOTIMU SAA SABA KAMILI MCHANA.





 XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX



NJIA NANE ZA KUEPUKA MIGOGORO MAKAZINI:

Imewahi kutokea ukawa na mgogoro na mfanyakazi mwenzako au hata kundi fulani la wafanyakazi wenzako,bosi wako nk?
Je,umewahi kushuhudia wafanyakazi wenzako wakiwa katika mgogoro au kutokuelewana kiasi kwamba wote hapo kazini mkakosa amani? Iwe ni wewe mwenyewe ulikuwa katika mgogoro au umeshuhudia wafanyakazi wenzako wakikosa kuelewana,ni imani yangu kwamba hukufurahishwa na jambo lile.
Tangu uchumi wa dunia ulipotetereka,tafiti mbalimbali zimeonyesha kwamba migogoro katika sehemu za kazi nayo imeongezeka maradufu.
Wana-saikolojia wanaihusisha hali hiyo na wasiwasi uliowakumba wafanyakazi wengi kuhusu kutokuwa na uhakika wa nini kitatokea kesho (fear of uncertainity)
Haishangazi kuona kwamba,leo hii,jinsi ya kutatua migogoro mbalimbali inayoweza kutokea makazini ni mojawapo ya majukumu makubwa ya mameneja,wakurugenzi na pia wafanyakazi wenyewe.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kwamba asilimia 24-60 ya muda makazini hutumika katika kutatua migogoro. Isitoshe,migogoro isiyokwisha katika sehemu za kazi matokeo yake huwa ni utendaji mbovu wa kazi, viwango hovyo vya utoaji wa huduma na kama ni sehemu ya biashara basi ni hasara au upotevu mkubwa wa hela.
Bila shaka ndio maana swali la ni hatua gani utazichukua ili kutatua migogoro mbalimbali inayoweza kujitokeza katika sehemu ya kazi ni mojawapo ya maswali yanayoulizwa zaidi wakati wa usaili(interview).
Leo ningependa tukumbushane mambo ya kufanya au kutofanya ili kuepuka migogoro makazini.
Mambo ya kufanya au kutofanya ili kuepuka migogoro yaweza kuwa mengi sana.Mimi nitaongelea 8 kwa leo.
Kama unazo njia nyingine mbalimbali ambazo pengine umewahi kuzitumia au unatambua kwamba zinasaidia katika kuepusha migogoro makazini;

Punguza Kuongea:

Maongezi ni jambo zuri. Lakini maongezi yakizidi huwa na tabia ya kuleta matatizo. Bahati mbaya zaidi ni kwamba punde maneno yakishakutoka,huwezi kuyarudisha.Utaomba msamaha,utaambiwa umesamehewa lakini ukweli ni kwamba ulichokisema kitabakia vichwani mwa mfanyakazi au wafanyakazi wenzako daima milele.
Jitahidi kufikiri kwanza kabla ya kuongea.Njia pekee ya kuweza kufanya hivyo ni kuongea taratibu na kwa mpangilio.Kwanza utasikika vizuri zaidi na pili utaepuka migogoro inayoanzia kwenye maneno.

Epuka Umbea:

Umbea na majungu ni chanzo kikubwa cha migogoro makazini. Sasa kama wewe ni mwanaume usidhanie kwamba hili halikuhusu. Umbea na majungu ni kwa wanaume na wanawake ingawa kuna tofauti kidogo za kitakwimu linapokuja suala la nani zaidi.Kwa vyovyote vile jiepushe na umbea au majungu kuhusu mfanyakazi au wafanyakazi wenzako.Jitahidi kufanya kazi yako kwa bidii na maarifa. Isitoshe huo ndio mwanzo wa kuheshimika.Hautoheshimika kwa kuwa msambazaji wa maneno ya uongo na matukio ya kutunga.

Subiri,tafakari kisha tenda:

 Makazini,kama zilivyo sehemu zingine ambazo binadamu hukutana,kupishana,kutofautiana kimavazi na kimawazo,huwa inatokea. Watu hukosa kuelewana.Inapotokea hivyo usikurupuke katika kuelezea malalamiko yako,mawazo yako au hata maoni yako.
Unapojipa muda wa kutafakari unachotaka kukisema au kurekebisha, unajipa nafasi ya kuwa sahihi zaidi mara utakapoamua kutenda. Fanya utafiti wa kina kabla ya kusema.Kwa kufanya hivyo utaheshimika zaidi na pia utaepusha migongano isiyo ya lazima.Nasema isiyo ya lazima kwa sababu naamini kwamba wakati mwingine mashauri hujitokeza kwa nia njema ya kuwekana sawa.

Sikiliza,usibishe:

  •  Imeshawahi kukutokea mfanyakazi mwenzako au bosi wako akakujia juu na kukulalamikia kwa kosa au kitu ambacho hujui chanzo wala mwisho wake na zaidi unaamini kabisa hujakosea wala kutenda jambo lolote baya? Hali hiyo inapokutokea huwa unafanya nini? Wengi wetu huwa tunaanza kwa kubisha na kujaribu kwa nguvu zetu zote kuhakikisha kwamba anachokisema mfanyakazi mwenzako au bosi wako sio kweli bali uongo mtupu.
Bahati mbaya njia hii mara nyingi hutufikisha pabaya zaidi. Wakati mwingine watu hurushiana hata ngumi! Badala yake sikiliza kwa makini unachotuhumiwa nacho na kisha taratibu sema “Nasikitika kusikia kwamba unadhani mimi ndiye niliye…”.Kisha mueleze mwenzio au bosi wako ukweli au unachokijua kuwa ukweli. Mara nyingi ukishampa mtu nafasi ya kusema kila kitu kilichoko moyoni mwake, hasira humpotea na akili timamu hurejea na hivyo mazungumzo yenye kujenga huwezekana.

Weka nukuu ya kila kitu:

  •  Binadamu wa kawaida ana mambo chungu mbovu kichwani kwake. Sio rahisi kukumbuka kila kitu kinachotokea iwe ni kazini, mitaani na hata majumbani. Kwa bahati mbaya mambo mengi yanayotokea kazini huwa yana thamani kubwa zaidi ya kukumbukwa. Jitahidi kuweka kumbukumbu ya kila kitu unachokiona,ulichoambiwa na wakuu wako wa kazi,mfanyakazi/wafanyakazi wenzako nk. Hiyo itakusaidia siku mgogoro utakapokuwa unafumuka. Kumbukumbu sahihi zitasema ukweli na pia zitaonyesha jinsi gani ulivyo makini katika kazi yako.Kumbukumbu sahihi zitakuepusha na mgogoro usio wa lazima baina yako na mfanyakazi mwenzako au hata utawala wa sehemu yako ya kazi.

Weka mipaka:

  • Kila binadamu ana mipaka yake.Kama hauna basi nakushauri uanze leo kujiwekea mipaka. Kwa upande wangu mojawapo ya mipaka ambayo huwa sina uvumilivu nayo sana mtu anapoivuka ni “unafiki”.Sipendi mtu/watu wanafiki”.Una jambo unataka kuliongelea kuhusu mimi,basi jitahidi tu kuniambia bila kuficha na kusemeasemea pembeni. Katika maeneo ya kazi ni muhimu kujiwekea mipaka ya mahusiano ya kikazi. Tambua majukumu yako,tambua wajibu wako.Majukumu yaw engine na wajibu wao,waachie wenyewe. Kumbusha majukumu na wajibu kama nafasi yako inakuruhusu kufanya hivyo.

Heshima na ubinadamu:

  •  Sasa niliposema hapo juu kwamba weka mipaka sikumaanisha kwamba uishi katika “dunia ya peke yako” mbele ya wafanyakazi wenzako. Jitahidi kuwa na mahusiano bora kabisa na wafanyakazi wenzako.Wajulie hali,wasalimie,wasaidie inapobidi,shiriki katika kila shughuli ya kazini(ndani na nje ya sehemu ya kazi).Usije ukaacha kushiriki shughuli kama misiba,harusi,ubarikio nk.Kumbuka maisha ni kushirikiana.


Usijaribu kuwabadili
wenzako,badilika mwenyewe:
Wapo binadamu ambao kila kukicha wao hujaribu kuwabadilisha wenzao? Kama wewe ni miongoni mwa watu wa namna hiyo,nasikitika kukuambia kwamba kazi kubwa ipo mbeleni mwako. Sio jambo rahisi kumbadili mtu. Ni sawa kabisa na kupoteza muda. Badala yake,jaribu wewe kubadilika.Kama mfanyakazi mwenzako ni ile aina ya watu wanaopenda kusifiwa sifiwa,msifu kisha ishia zako.Kwani utapungukiwa na nini?
Mwisho,kumbuka mambo kadhaa ya msingi.Upendo, heshima na uvumilivu. Mambo hayo ndio msingi wa kwanza wa mafanikio na siri ya kuepusha migogoro makazini. Mpende kila mtu(hata kama unadhani hapendeki),mheshimu kila mtu bila kusahau kujiheshimu wewe mwenyewe.Jitahidi kuwa mvumilivu.Kila mtu anastahili kuvumiliwa, ukiwemo wewe na mimi pia. Kazini ni sehemu ya kujitafutia riziki,kujenga mahusiano bora ya kibinadamu,kujiendeleza,kuwaendeleza wengine na muhimu zaidi kujifunza na siyo sehemu ya kutengeneza migogoro. Asanteni Tuonane kesho muda kama huu.


MWISHO